Acts 16:12-40

12 aKutoka huko tukasafiri hadi Filipi, mji mkuu wa jimbo hilo la Makedonia, uliokuwa koloni ya Warumi. Nasi tukakaa huko siku kadhaa.

13 bSiku ya Sabato tukaenda nje ya lango la mji kando ya mto, mahali ambapo tulitarajia tungepata mahali pa kufanyia maombi. Tukaketi, tukaanza kuongea na baadhi ya wanawake waliokuwa wamekusanyika huko. 14 cMmoja wa wale wanawake waliotusikiliza aliitwa Lidia, mfanyabiashara wa nguo za zambarau, mwenyeji wa mji wa Thiatira, aliyekuwa mcha Mungu. Bwana akaufungua moyo wake akaupokea ujumbe wa Paulo. 15 dBasi alipokwisha kubatizwa yeye na watu wa nyumba yake, alitukaribisha nyumbani kwake akisema, “Kama mmeona kweli mimi nimemwamini Bwana, karibuni mkae nyumbani mwangu.” Naye akatushawishi.

Paulo Na Sila Watiwa Gerezani

16 eSiku moja, tulipokuwa tukienda mahali pa kusali, tulikutana na mtumwa mmoja wa kike ambaye alikuwa na pepo wa uaguzi. Naye alikuwa amewapa mabwana zake mapato makubwa ya fedha kwa ubashiri. 17 fHuyu msichana alikuwa akimfuata Paulo na sisi akipiga kelele, “Watu hawa ni watumishi wa Mungu Aliye Juu Sana, wao wanawatangazieni njia ya wokovu.” 18 gAkaendelea kufanya hivi kwa siku nyingi, lakini Paulo akiwa ameudhika sana, akageuka na kumwambia yule pepo mchafu, “Ninakuamuru katika jina la Yesu Kristo, umtoke!” Yule pepo mchafu akamtoka saa ile ile.

19 hBasi mabwana wa yule mtumwa wa kike walipoona kuwa tumaini lao la kuendelea kujipatia fedha limetoweka, wakawakamata Paulo na Sila wakawaburuta mpaka sokoni mbele ya viongozi wa mji. 20 iBaada ya kuwafikisha mbele ya mahakimu wakawashtaki wakisema, “Hawa watu wanaleta ghasia katika mji wetu, nao ni Wayahudi. 21 jWanafundisha desturi ambazo sisi raiya wa Kirumi hatuwezi kuzikubali au kuzitimiza.”

22 kUmati wa watu waliokuwepo wakajiunga katika kuwashambulia Paulo na Sila na wale mahakimu wakaamuru wavuliwe nguo zao na wachapwe viboko. 23 lBaada ya kuwachapa sana, wakawatupa gerezani na kumwagiza mkuu wa gereza awalinde kikamilifu. 24 mKufuata maelekezo haya, yule mkuu wa gereza akawaweka katika chumba cha ndani sana mle gerezani, na akawafunga miguu yao kwa minyororo.

25 nIlipokaribia usiku wa manane, Paulo na Sila walikuwa wakiomba na kuimba nyimbo za kumsifu Mungu, nao wafungwa wengine walikuwa wakiwasikiliza. 26 oGhafula pakatokea tetemeko kubwa la ardhi, hata msingi wa gereza ukatikisika. Mara milango ya gereza ikafunguka na ile minyororo iliyowafunga kila mmoja ikafunguka. 27 pYule mkuu wa gereza alipoamka na kuona milango ya gereza iko wazi, akachomoa upanga wake akataka kujiua, akidhani ya kuwa wafungwa wote wametoroka. 28Lakini Paulo akapiga kelele kwa sauti kubwa, akasema, “Usijidhuru kwa maana sisi sote tuko hapa!”

29Yule askari wa gereza akaagiza taa ziletwe, akaingia ndani ya kile chumba cha gereza, akapiga magoti akitetemeka mbele ya Paulo na Sila. 30 qKisha akawaleta nje akisema, “Bwana zangu, nifanye nini nipate kuokoka?”

31 rWakamjibu, “Mwamini Bwana Yesu Kristo, nawe utaokoka, pamoja na watu wa nyumbani mwako.” 32Wakamwambia neno la Bwana yeye pamoja na wote waliokuwako nyumbani mwake. 33 sWakati ule ule, yule mkuu wa gereza akawachukua, akawaosha majeraha yao, kisha akabatizwa yeye pamoja na wote waliokuwa nyumbani mwake bila kuchelewa. 34 tAkawapandisha nyumbani mwake akawaandalia chakula, yeye pamoja na nyumba yake yote wakafurahi sana kwa kuwa sasa walikuwa wamemwamini Mungu.

35Kulipopambazuka wale mahakimu wakawatuma maafisa wao kwa mkuu wa gereza wakiwa na agizo linalosema, “Wafungue wale watu, waache waende zao.” 36 uMkuu wa gereza akamwambia Paulo “Mahakimu wameagiza niwaache huru, kwa hiyo tokeni na mwende zenu kwa amani.”

37 vLakini Paulo akawaambia wale maafisa, “Wametupiga hadharani bila kutufanyia mashtaka na kutuhoji, nao wakatutupa gerezani, hata ingawa sisi ni raiya wa Rumi. Nao sasa wanataka kututoa gerezani kwa siri? Hapana! Wao na waje wenyewe watutoe humu gerezani.”

38 wWale maafisa wakarudi na kuwaambia wale mahakimu maneno haya, wakaogopa sana walipofahamu kuwa Paulo na Sila ni raiya wa Rumi. 39 xKwa hiyo wakaja wakawaomba msamaha, wakawatoa gerezani, wakawaomba waondoke katika ule mji. 40 yBaada ya Paulo na Sila kutoka gerezani walikwenda nyumbani kwa Lidia, ambapo walikutana na wale ndugu walioamini, wakawatia moyo, ndipo wakaondoka.

Copyright information for SwhNEN